Suarez Kuikosa Copa America.
Mshambuliaji nyota wa timu ya Barcelona Luis Suarez atakuwa nje ya michuano ya mataifa ya Amerika ya kusini maarufu kama Copa America kutokana na kuendelea kutumikia adhabu ya kukosa michezo tisa kufuatia kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chielini kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka jana .
Suarez atalazimika kuwatazama wenzie kwenye televisheni kutokana na adhabu hiyo ambayo imebakiza michezo saba kabla ya kumalizika .
Uruguay inayofundishwa na kocha mkongwe Oscar Washington Tabarez italazimika kumtegemea mshambuliaji wa PSG Edinson Cavani kwenye idara ya ushambuliaji huku ikimkosa pia Diego Forlan ambaye amestaafu kucheza timu ya taifa .
Forlan ambaye alistaafu mwezi machi mwaka huu amesema kuwa anaamini Uruguay ina wachezaji wazuri na wenye uwezo ambao wataziba pengo la Suarez na kufanya vizuri kwenye michuano ya mwaka huu .
Uruguay ndio mabingwa watetezi wa michuano ya Copa America ambayo waliitwaa mwaka 2011 nchini Argentina ambako waliwafunga Paraguay kwenye fainali na wanaingia kwenye michuano ya mwaka huu kama moja ya timu zinazopewa nafasi ya kufanya vizuri