REALMADRID YAMTIMUWA CARLO ANCELOTTI

.
Hatimaye miamba ya soka nchini Hispania Real Madrid imemtimua kocha wa timu hiyo Carlo Ancelotti baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa misimu miwili.
Kocha huyo raia wa Italia, aliiongoza Madrid kutwaa taji la kombe la Hispania kabla ya kuibebesha miamba hiyo taji la kumi la klabu bingwa barani Ulaya. Pamoja na mafanikio hayo aliyoyapata msimu uliopita, mwaka huu haukuwa mzuri kwa vijana hao wa Benabeu baada ya kuambulia patupu kwa kukosa hata kombe moja japokuwa kikosi cha timu hiyo kinatajwa kuwa cha gharama ya juu. Hasira za viongozi wa klabu hiyo ziliongezeka baada ya kutupwa nje na Juventus katika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya huku wapinzani wao wakubwa Barcelona ikinyakuwa taji la ligi kuu na kutinga fainali ya klabu bingwa na kombe la Hispania. Rais wa Madrid Florentino Perez amewaambia waandishi wa habari kuwa haikuwa rahis kumtema kocha huyo na kuongeza kuwa kocha mpya atateuliwa wiki ijayo.