Akizungumza jana, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema mwaka huu CCM itakuwa na ushindani mkali kuliko ilivyowahi kutokea kwenye uchaguzi wowote wa nyuma.
Wasomi na wachambuzi wa siasa wamesema Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameona mbali kuwataka viongozi wa chama hicho kuteua mgombea wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama wakisema bila kufanya hivyo wataangushwa na mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza jana, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha
(Rucu), Gaudence Mpangala alisema mwaka huu CCM itakuwa na ushindani
mkali kuliko ilivyowahi kutokea kwenye uchaguzi wowote wa nyuma.
Alisema ushindani huo unatokana na kuwapo kwa mgombea urais wa Ukawa unaoundwa na vyama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
“Vyama hivyo vimeamua kushirikiana kusimamisha
mgombea mmoja kwenye nafasi ya urais, ubunge na udiwani, ushirikiano huo
utatoa upinzani mkali kwa CCM,” alisema Mpangala.
Alisema CCM wameliona hilo na ndiyo maana Rais
Kikwete ameona ni muhimu awaeleze wana CCM kwamba wanatakiwa kuchagua
viongozi wanaokubalika na wananchi walio wengi, vinginevyo watashindwa.
“Yale mambo ya zamani ya kila kundi kuwa na
mgombea wake yakirudiwa hivi sasa yatakigharimu chama hicho, wanatakiwa
kuungana na kuweka mtu anayekubalika bila kujali makundi,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo pia alisema Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu utakuwa na tofauti kubwa na chaguzi zilizopita, hivyo lazima
wapate mgombea maarufu.
Akitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995
alisema: “Katika kipindi hicho Mkapa (Benjamin) hakuwa akifahamika sana
ukilinganisha na wana-CCM wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo lakini
alishinda na kuwa rais. Mwaka huu wakijaribu kufanya hivyo wataanguka
vibaya, hali ya kisiasa imebadilika,” alisema.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, viashiria
vinaonyesha kuwa vyama vya upinzani vinazidi kuwa na nguvu mwaka hadi
mwaka, akitaja Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita kama mfano...
“Hata mgombea wa urais wa CCM, 2010 alipata kura chache ikilinganishwa
na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Hii ina maana vyama vya upinzani vinakua
kwa kasi,” alisema.
Alisema kukithiri kwa rushwa na umaskini katika
jamii kumewakatisha tamaa wananchi hivyo watahitaji kiongozi mwenye
uwezo kupunguza matatizo hayo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel
Malya alisema Rais Kikwete anafahamu kuwa chama hicho kisipoweka
wagombea wanaokubalika kitaanguka kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Kikwete ameliona hilo na wanachama wenzake
wafahamu kuwa huu si wakati wa kuweka mtu wao, bali mtu anayekubalika na
wananchi walio wengi,” alisema.